Jumanne, 1 Julai 2014

KUTUNZA KUMBUKUMBU ZA TAIFA NI MUHIMU


Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue (mwenye miwani), akiwa na Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma. Balozi Sefue alitembelea Kituo cha Taifa cha Uhifadhi wa Kumbukumbu.


Ni lazima kutunza Kumbukumbu na Nyaraka za nchi yetu vizuri ili vizazi vijavyo viweze kuelewa uhalisia wa historia ya Nchi na visitulaumu.


Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Y. Sefue alisema hayo alipotembelea Kituo cha Taifa cha Uhifadhi wa Kumbukumbu (NRC), mkoani Dodoma.

“Hatuwezi kupewa na kujifunza mambo yaliyotokea katika nchi yetu kwa njia ya mdomo kutoka kizazi kimoja hadi kingine” Balozi Sefue alisema na kuongeza kutegemea njia ya kusimuliwa masuala ya historia ya Nchi ipo siku itapotea na haitakua halisi kwa sababu matukio yanayotokea ni mengi na kukumbuka yote sio rahisi.

Balozi Sefue alisisitiza kuwa vizazi vinabadilika hivyo historia lazima itunzwe vizuri katika maandishi kwa marejeo ili kupata ukweli halisi wa yaliyotokea siku za nyuma.

Awali, Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma Bw. George D. Yambesi akimkaribisha Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Sefue alisema Serikali iliamua kuwa na Kituo cha Taifa cha Uhifadhi wa Kumbukumbu (NRC) tuli kutoka Taasisi mbalimbali za Umma kwa sababu Taasisi hizo pamoja na Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa zilikosa nafasi ya kutunzia kumbukumbu hizo.

“Lengo la kujenga Kituo cha Taifa cha Kumbukumbu na Nyaraka linatokana na umuhimu wa kukusanya, kuchambua, kutunza na kuhifadhi kumbukumbu za Serikali ili kulinda urithi andishi na historia ya Taifa letu” Bw. Yambesi alisema.

Bw. Yambesi aliongeza sababu nyingine za kuwa na kituo hicho ni  Serikali kulinda haki za Raia wake kwa kutunza taarifa mbalimbali zinazohusu maslahi ya Taifa kwa ujumla kama vile kumbukumbu zinazohusu masuala ya haki za kiutumishi, haki ya ardhi, haki za mahakama, taarifa za afya, fedha, mgawanyo wa raslimali za Taifa.

Aliongeza matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika Ofisi za Umma kumeilazimu Serikali kuwa na kituo cha kisasa cha kutunza na kuhifadhi taarifa zinazozalishwa kwa njia ya TEHAMA.

Katibu Mkuu Utumishi Bw. Yambesi alisema kituo hicho kitaziondolea Taasisi za serikali tatizo la mlundikano wa kumbukumbu tuli na hivyo kupunguza gharama za kulipia nafasi za kutunzia kumbukumbu zisizotumika, pia kurahisisha upatikanaji wa kumbukumbu zilizotumika kwa
maamuzi mbalimbali yaliyofanyika na Serikali kwa maslahi ya
Taifa.

Kituo hicho kitawezesha watalaam wa ndani na nje ya nchi kufanya tafiti mbalimbali kwa maendeleo ya Taifa letu na kuwa kituo kikuu cha taarifa muhimu za Serikali zilizotumika katika kufanya maamuzi mbalimbali hususan yaliyo na tija kwa Taifa.


Katibu Mkuu Ofisi ya Rais-Utumishi Bw. Yambesi alisema ujenzi wa kituo hicho ambacho kimeanza kutumika umeongeze uwezo wa Idara katika kuhifadhi kumbukumbu na nyaraka za Taifa kwa asilimia 250 yaani kutoka kuhifadhi mafaili 200,000 hadi 700,000 (maboksi 55,280) hivyo kuokoa nafasi ya mita za mraba 77,700 zilizokuwa zikitumika na Taasisi za
Serikali kuhifadhia kumbukumbu tuli.

Ujenzi wake umefanyika kwa ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania na Washirika wa Maendeleo ambao ni Benki ya Dunia, DFID na Kanada.


Historia inaonyesha Tanzania baada ya kupata Uhuru, suala la utunzaji wa kumbukumbu katika Ofisi za Serikali lilitollewa  Waraka wa Rais Namba 7 wa Mwaka 1963 juu ya utunzaji bora wa Kumbukumbu na Nyaraka za Serikali. Mwaka 1965 Sheria ya Nyaraka za Taifa ilitungwa na Bunge ikiwa na jukumu la kulinda na kuhifadhi urithi andishi wa Taifa. Sheria hii pia ilianzisha rasmi Idara ya Nyaraka za Taifa. Mnamo mwaka 1999, chini ya Programu ya Mabadiliko Katika Utumishi wa Umma(PSRP), iliamuliwa sehemu ya kumbukumbu iliyokuwa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma iunganishwe na Idara ya Nyaraka iliyokuwa chini ya Wizara ya Elimu na kuunda Idara ya Kumbukumbu na Nyara za Taifa. Mnamo mwaka 2002, Bunge la Jamhuri ya Muungano lilitunga Sheria ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa namba 3 ya mwaka 2002.

(BK)

Hakuna maoni: